Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Mujtaba Huseini Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika ujumbe wake kwa mnasaba wa Wiki ya Umoja, baada ya kutoa pongezi kwa kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.), Mtume wa mwisho, na Imam Ja’far Sadiq (a.s.), alisema kuwa; mpango wa watu wenye nia mbaya na maadui wa Uislamu ni kuibua na kukuza tofauti kwa ajili ya kuudhoofisha na kuutawala Umma wa Kiislamu.
Aidha, akirejelea kuanguka kwa vinyago vya udanganyifu vilivyoficha nyuso za kihalifu za Marekani, alisisitiza ulazima wa kuungana Umma wa Kiislamu, kuteteana mbele ya ukafiri, pamoja na kuongeza ushirikiano katika masuala mbalimbali ya kimaada na kiroho. Akizungumza na watawala wa nchi za Kiislamu, alisisitiza: “Watawala wahalifu wa Marekani na utawala bandia wa Kizayuni ni maadui walioapa kupambana na umoja wa Kiislamu na Umma wote wa Kiislamu, wakiwemo watu wa Asia Magharibi na Afrika Kaskazini. Kwa hiyo, mtambueni adui wenu wa kweli na pingeni njama yake.”
Aidha, akirejelea kutekelezwa kwa kiwango cha kuridhisha mafundisho ya umoja ya mfumo wa Kiislamu ndani ya Iran, kwa mara nyingine aliwasihi wananchi wote kutoruhusu kabisa kutokea tofauti yoyote miongoni mwao.
Matini ya ujumbe wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kama ifuatavyo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu
مُحَمَّدٌ رَسُولُ اللهِ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِّدَّاءُ عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاءُ بَيْنَهُمْ
Natoa pongezi kwa taifa tukufu la Iran na Umma mkubwa wa Kiislamu kufuatia siku za kuzaliwa yule mwenye uwepo uliobarikiwa, nuru kuu kabisa, mbora wa viumbe, taa yenye kung’aa, mteule wa Mwenyezi Mungu, mji wa elimu, mwenye rehema kwa walimwengu, Mtume Mtukufu wa Uislamu, Muhammad (s.a.w.w.), pamoja na mwanawe mtukufu na mwenye asili njema, hoja thabiti ya Mwenyezi Mungu, Imam Ja’far Sadiq (a.s.).
Tangu wakati jua la uwepo wa Mtume wa mwisho lilipochomoza ndani ya Makkah Tukufu, upeo wa saada ya mwanadamu, ambayo inategemea ukamilifu wa kumtumikia na kumtii Mwenyezi Mungu Mtukufu, ulipata mwangaza mpya. Roho za Mitume, Malaika watukufu wa Mwenyezi Mungu zilijawa na furaha, huku mashetani miongoni mwa majini na wanadamu wakiuma vidole vyao kwa hasira, majuto na huzuni.
Hii ni kwa sababu kiumbe bora zaidi wa Mwenyezi Mungu katika walimwengu wote wasio na idadi wa uumbaji alikuwa akiingia katika ulimwengu wa ardhi, na hivi karibuni, akiwa amevalishwa vazi la Utume na kuwa Mtume wa mwisho, huku akiwa ameshikilia Qur’ani Tukufu na kubeba jukumu la kuwaongoza wanadamu kwa kila upande, alikuwa akienda kuweka mwelekeo wa msafara mkubwa wa wanadamu kuelekea katika kumwabudu Mwenyezi Mungu na ukamilifu wa kuelekea kwa Mwenyezi Mungu.
Maisha ya Mtukufu huyo na wasii wake Ma’asumina kwa ujumla wake, ni somo la uongofu na ibada; somo la maarifa na mapenzi; somo la itikadi na jihadi; somo la maisha na tabia njema za mtu binafsi na za kijamii; somo la uaminifu na ukweli; somo la heshima na utu; somo la elimu na vitendo; somo la rehema na uthabiti; somo la uadilifu na haki; na somo la umoja na udugu.
Kadiri masomo haya yanavyofundishwa na kutekelezwa kwa ubora zaidi, ndivyo inavyokuwa rahisi zaidi kwa wanadamu kufikia kilele cha saada na heri.
Sisi tunaamini kwamba roho tukufu ya Mtume wa Rehema, pamoja na roho safi za Mawasii na Hoja wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na juu yao wote, daima zinawachunga, zinawaongoza na kuwahurumia Waislamu na jamii ya Kiislamu. Pale mmoja wa watoto wa baba huyu mwenye huruma na mtukufu anapofanya kosa, nyoyo zao huumia; na kila Waislamu wanapotekeleza mafundisho na maagizo yao, nyoyo zao tukufu hujawa na furaha.
Leo, Uislamu na watu wake, baada ya kuvuka vipindi vigumu na vyenye misukosuko na kupitia kupanda na kushuka kwingi tangu mwanzo wa Uislamu hadi leo, umefikia hatua ya hatima na yenye kuamua mustakabali. Leo, Waislamu wanaweza kutekeleza jukumu lenye athari kubwa na la kihistoria. Leo ni siku ambayo upeo wa ushindi wa mwisho wa haki dhidi ya batili, na wa Uislamu dhidi ya ukafiri, umekaribia kutimia kwa uhalisia zaidi kuliko katika vipindi vyote vilivyopita.
Sharti la kwanza la jambo hili muhimu ni umoja wa kauli wa Waislamu. Umoja wa Waislamu mbele ya ukafiri wa dunia ni mkakati wa Qur’ani na ni fundisho halisi kutoka katika Uislamu safi wa Muhammad (s.a.w.w.), wala si jambo la juu juu au la kupita. Maana ya umoja ni kwamba katika kiwango cha jumla cha jamii za Kiislamu, mambo yanayowaunganisha wote yawekwe kuwa mhimili na msingi.
Bila shaka, jitihada inapaswa kufanywa, kwa kuungwa mkono na hoja na kwa kuzingatia kikamilifu masharti yote ya udugu na kushirikiana, na kwa namna inavyotokana na mafundisho ya Qur’ani, kwa amani na utulivu kamili, ili maeneo ya tofauti yageuzwe kuwa maeneo ya ushirikiano.
Jambo lisilo na shaka ni kwamba kila Mwislamu katika jamii za Kiislamu, anapokabiliana na ukafiri wa dunia, anapaswa kuweka msingi wa Qur’ani wa «أَشِدَّاءُ عَلَى الْكُفَّارِ، رُحَمَاءُ بَيْنَهُمْ» kuwa mhimili wa fikra, kauli na matendo yake. Hivi ndivyo umoja na mshikamano wa Kiislamu unavyopatikana.
Pale ambapo mojawapo ya sehemu hizi mbili za ujumbe huu wa mbinguni itaondolewa katika utekelezaji wa Waislamu, nao watakuwa wamejitenga na nafasi hiyo ya heshima ambayo kwa haki waliipata katika mji wa Uislamu. Hii ni kanuni ambayo haina kinyume chake.
Kanuni hii ni miongoni mwa misingi na jumbe muhimu za Mapinduzi ya Kiislamu. Muda wa kufanyika kwa Wiki ya kwanza ya Umoja unarejea mwezi wa Esfand mwaka 1356 Hijria ya Shamsia, katika kipindi cha mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Pahlavi; wakati ambapo Kiongozi Mkuu mwenye heshima, shahidi — Mwenyezi Mungu autukuze zaidi utukufu wa cheo chake — alipokuwa uhamishoni katika mji wa Iran Shahr, alitoa wazo hili, na Shia na Sunni walilipokea kwa ukaribisho.
Mara tu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kwa busara ya mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu, Imam Khomeini — Mwenyezi Mungu aitukuze siri yake tukufu — “Wiki ya Umoja” ilifanywa kuwa rasmi.
Kwa fadhila za Mwenyezi Mungu Mtukufu, suala la umoja miongoni mwa wananchi wote wa taifa la Kiislamu limekuwa na mfano wenye mafanikio miongoni mwa watu wa Iran, na njama za maadui hazijaweza kuwa na athari kubwa katika kuuharibu umoja huo.
Lakini bila shaka, watu wenye nia mbaya daima wanauotea na kuuvizia wema huu mkubwa, kinachowapa matumaini ni kuibua na kukuza tofauti.
Tofauti za kiitikadi na kidini, ingawa ni sehemu muhimu ya lengo la maadui wa Uislamu, ambao wameweka matumaini makubwa katika kuzitumia, hawataridhika nazo pekee. Wanajitahidi pia kugeuza aina mbalimbali za tofauti za kikabila, kiutamaduni, kijamii, kiuchumi, kisiasa na kijiografia kuwa visingizio vya kuleta mifarakano miongoni mwa watu Waislamu nchini Iran na katika nchi nyingine yoyote ya Kiislamu.
Kwa njia hii, wanataka kutazama Umma wa Kiislamu ukipasuka vipande vipande na nguvu zake zikidhoofika, ili katika fursa inayofaa waweze kuutawala.
Maagizo ya Qur’ani Tukufu kuhusu jambo hili yameelezwa katika aya tukufu:
«وَلا تَنَازَعُوا فَتَفْشَلُوا وَتَذْهَبَ رِيحُكُمْ»
Kwa hiyo, mtu yeyote, katika nafasi yoyote, anayefanya jambo lolote linalosababisha mifarakano miongoni mwa Waislamu na kuleta mzozo katika jamii ya Waislamu, iwe anajua au hajui, iwe kwa kutaka au bila kutaka, anakuwa amesaidia kutekeleza lengo la maadui wa Uislamu.
Na katika zama hizi, mtu anawezaje kulihusisha jambo kama hilo na ujinga au uzembe wake, wakati ambapo leo madhalimu duniani, na Marekani ya kihalifu ikiwa katika mstari wa mbele, wameondoa kutoka kwenye nyuso zao mbaya vinyago vya udanganyifu na vya kubuni vilivyokuwa vikificha malengo yao mabaya ya kikoloni na mipango yao ya kiistikbari na ya kutaka kutawala, wamevua glovu zao za zenye kudanganya, na wameionesha dunia nzima makucha yao yaliyolowa damu?
Sasa ni wakati wa Waislamu kutafakari na kuyaangalia matukio kwa umakini zaidi.
Je, kama Waislamu wangekuwa mkono mmoja, wakikunja ngumi yao kwa nguvu na mshikamano, watu wa Palestina wangekuwa wanakabiliwa na ukosefu huu wa ulinzi, wakifanyiwa dhuluma na jinai na wavamizi?
Na je, kama mataifa na serikali zinazopatikana katika mwambao wa Ghuba ya Uajemi zingeimarisha umoja wao chini ya bendera ya Uislamu, watu hawa wasio na utambulisho na mafisadi wangeweza kuthubutu, kutoka maelfu ya kilomita mbali, kutamani ardhi na mali zao?
Ushauri wangu wa kusisitiza na wa mara kwa mara kwa watawala wa nchi za Kiislamu, hususan nchi za eneo la Asia Magharibi na mwambao wa Ghuba ya Uajemi, ni huu: Mtambueni adui wenu wa kweli na mfahamu mpango wake, kisha pingeni njama zake.
Tiba ya matatizo ya Umma wa Kiislamu ni umoja wa kauli, urafiki na kushirikiana katika njia ya kheri na wema.
Watawala wahalifu wa Marekani na utawala bandia wa Kizayuni ni maadui walioapa kuupiga vita umoja na urafiki huu. Wao si maadui wa Jamhuri ya Kiislamu, taifa la Iran na mhimili mkubwa wa Muqawama wa Kiislamu pekee; bali wanauadui na Umma wote wa Kiislamu, wakiwemo watu wa Asia Magharibi na Afrika Kaskazini.
Na katika jambo hili, hata watawala wa nchi hizi, ambao wengi wao wanahesabiwa kuwa washirika wao, hawako nje ya jambo hilo; kama ambavyo katika kumbukumbu zenu na zetu za karibu bado kuna mifano ya kutoheshimu waziwazi na kutumia maneno machafu dhidi ya baadhi ya viongozi wa nchi za Kiislamu kutoka kwa marais wa madola ya kibeberu.
Somo muhimu la umoja na kutokugombana ni somo la kwanza la mfumo wa Uislamu kuhusu namna ya kukabiliana na adui na rafiki. Lakini somo la pili ni kuteteana mbele ya ukafiri, na somo la tatu ni aina mbalimbali za ushirikiano na kuongeza nguvu kwa pamoja katika masuala mbalimbali ya maisha ya kimaada na kiroho ya Waislamu, katika nyanja za utajiri, usalama, elimu na maendeleo.
Mwisho wa njia hii ni kufikia ustaarabu mpya wa Kiislamu.
Kwa hiyo, umoja miongoni mwa Waislamu ndio jiwe la msingi la kufikia ustaarabu mtukufu na wenye nguvu wa Kiislamu. Mfumo huu wa dhana na fikra, ambao ndani yake imo ndoto yetu kwa ajili ya ulimwengu wa Kiislamu, kwa upande wake umetimia kwa kiwango cha kuridhisha nchini Iran. Na kwa mara nyingine, ushauri wa mtumishi huyu kwa wananchi wote ni kwamba kwa vyovyote vile wasiruhusu kutokea tofauti yoyote miongoni mwao.
Mwisho, ninatumaini kwamba kwa shafaa ya Mtume Mtukufu na Ahlul-Baiti wake watakatifu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na juu yao, kivuli cha rehema na baraka za fadhila za Mwenyezi Mungu kitazifunika jamii za Kiislamu, na kwamba wao, siku baada ya siku, chini ya kivuli cha kutekeleza amri za Mwenyezi Mungu, wataendelea kupanda zaidi na zaidi ngazi za maendeleo na heshima.
Wassalaamu ‘alaykum warahmatullahi wabarakaatuh.
Sayyid Mujtaba Husaini Khamenei
8/ Shahrivar/ 1405
17/ Rabiul-Awwal/ 1448
Maoni yako